*NAFASI YA CEO NA ZINGINE ZOTE ZA MENEJIMENTI NDANI YA KLABU YA YANGA ZINAPASWA KUJAZWA UPYA KABLA YA KUANZISHWA KAMPUNI YA KIBIASHARA YA YANGA*
Taarifa ya Kamati ya Utendaji ya Yanga jana usiku kwamba imekubali maombi ya Mtendaji Mkuu wa Klabu, Senzo Hammilton Mazingiza, kutoendelea na nafasi yake baada ya mkataba wake kumalizika leo tarehe 31.7.2022 umenifanya kuipitia Katiba ya Yanga (Yenye Marekebisho ya Mwaka 2021) na kubaini yafuatayo:-
1. Uongozi wa Yanga chini ya Rais Injinia Hersi Ally Said unapaswa kuunda timu mpya ya menejimenti yenye ajira ya kudumu kwa mujibu wa Ibara ya 37.
2. Timu ya menejimenti itaundwa na Mtendaji Mkuu (CEO) na Wakurugenzi saba ambao ni Mkurugenzi wa Sheria na Katiba, Mkurugenzi wa Mipango, Fedha na Utawala, Mkurugenzi wa Uwekezaji na Masoko, Mkurugenzi wa Michezo, Mkurugenzi wa Mahusiano ya Wanachama na Mashabiki, na Mkurugenzi wa Mifumo ya Tehama na Mawasiliano ya Wanachama na Mashabiki.
3. Nafasi hizo zinajazwa kwa kutangazwa ili kupata watu wenye sifa ikiwemo elimu ya chini ni shahada ya kwanza ya chuo kikuu.
4. Hii ina maana kwamba nafasi zote za menejimenti ya Yanga lazima zijazwe upya kuanzia ngazi ya Mtendaji Mkuu (CEO) kwani ni nafasi ya ajira ya kudumu na sio ya mkataba.
5. Watendaji wote lazima wawe ni wanachama wa Yanga isipokuwa Kamati ya Utendaji itaona inafaa kuajiri mtaalam kutoka nje, kwenye nafasi mojawapo, kigezo cha uanachama hakitazingatiwa.
6. Timu ya menejimenti itaongozwa na Mtendaji Mkuu wa Yanga ambaye kazi zake mahususi zimetajwa katika Ibara ya 37 (5) na 38 (1) - (9) zikiwemo utekelezaji wa maamuzi ya Mkutano Mkuu, Kamati ya Utendaji na vyombo vingine vya Yanga, kutunza vitabu vya hesabu za fedha za klabu akiwa ni ofisa masuuli wa klabu, kusimamia menejimenti ya klabu ikiwemo kuajiri watumishi wa kawaida, mwandishi wa kumbukumbu za Mkutano Mkuu na Kamati ya Utendaji na kuzihifadhi, kutayarisha mipango ya bajeti na taarifa za fedha za klabu, na kujibu hoja za ukaguzi wa fedha.
7. Mtendaji Mkuu atawajibika kutoa taarifa ya uendeshaji wa makampuni kwa kamati ya utendaji. Makampuni hayo ni kama ile inayotajwa na Katiba katika Ibara ya 56 ambayo ni ya kibiashara itakayosajiliwa kama kampuni binafsi (private company) yenye ukomo wa dhima (limited liability) ambayo klabu itamiliki hisa zisizopungua asilimia hamsini na moja (51%) ya hisa zote na wawekezaji watamiliki hisa zisizozidi arobaoni na tisa (49%).
8. Klabu itateua wakurugenzi wenye sifa sitahiki kuhudumu katika Bodi ya Wakurugenzi ya kampuni husika. Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi atatoka upande wa klabu. Bodi hiyo itaundwa na wawakilishi kutoka klabu na wawekezaji.
9. Bodi itakuwa pia na wajumbe kutoka klabu ambao ni Rais wa Klabu na Mtendaji Mkuu wa Klabu ambao watakuwa na nafasi mbili (2) za kudumu. Aidha, kutakuwa na wajumbe wawili (2) watakaoteuliwa na Kamati ya Utendaji na mjumbe mmoja (1) atakayeteuliwa na Bodi ya Wadhamini wa klabu ambao wataungana na wengine wanne (4) kutoka upande wa wawekezaji.
10. Kampuni itakayoundwa itakuwa ni chombo maalum cha klabu kitakachokuwa na dhamana ya kufanya biashara ambayo Yanga itaona inafaa kwa malengo ya kuisaidia Yanga kiuchumi katika kufikia malengo yake kwa weledi wa hali ya juu.
HIVYO NAFASI ZOTE ZA MENEJIMENTI NDANI YA YANGA ZINAPASWA KUJAZWA UPYA KWA MUJIBU WA IBARA YA 37 KATIBA NA NDIYO KAZI ATAKAYOFANYA KAIMU CEO, WAKILI MSOMI SIMON PATRICK, CHINI YA KAMATI YA UTENDAJI IKIONGOZWA NA RAIS INJINIA HERSI ALLY SAID.
Share this page with your family and friends.